Mwanzo › Masomo ya Biblia ya kila siku › Machi 2027 › 21 Machi
Kalenda ya Kikatoliki
Masomo ya Misa (Kikatoliki) — 21 Machi 2027
Jumapili · Juma Kuu
Sikukuu na watakatifu
Dominika ya Matawi ya Mateso ya Bwana
Dominika · Rangi ya liturujia: nyekundu
Masomo ya siku
Injili ya maandamano
au: Yn 12:12–16
1Wakati huo walipokuja Yerusalemu, walipokaribia Besthfage na Bethania, katika Mlima wa Mizeituni, Yesu aliwatuma wawili miongoni mwa wanafunzi wake 2na aliwaambia, “Nendeni katika kijiji kinachokabiliana nasi. Mara mtakapoingia humo, mtamkuta mwanapunda ambaye hajapandwa. Mfungueni na mmlete kwangu. 3Na kama yeyote akiwaambia, 'Kwa nini mnafanya hivi'?, mnapaswa kusema, 'Bwana anamhitaji na mara atamrudisha hapa'.” 4Walikwenda na kumkuta mwanapunda amefungwa nje mlangoni kwenye mtaa ulio wazi, nao walimfungua. 5Na baadhi ya watu walikuwa wamesimama pale na waliwaambia, “Mnafanya nini, kumfungua mwanapunda huyo?” 6Waliwaambia kama Yesu alivyowaambia, na watu wakawaacha waende. 7Wanafunzi wawili walimleta mwanapunda kwa Yesu na walitandika mavazi yao juu yake ili Yesu aweze kumpanda. 8Watu wengi wakatandika mavazi yao barabarani, na wengine wakatandika matawi waliyoyakata kutoka mashambani. 9Wale waliokwenda mbele yake na wale waliomfuata walipiga kelele, “Hosana! Amebarikiwa anayekuja kwa jina la Bwana. 10Ubarikiwe ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi! Hosana kwa aliye juu”
Somo la kwanza
4Bwana Yahwe amenipa mimi lugha kama wale wanayofundishwa, ili kwamba nizungumze maneno ya kudumisha kwa yeye aliyechoka; huniamsha mimi asubuhi kwa asubuhi; huyaamsha masikio yangu kama wale wanofundisha. 5Bwana Yahwe amefungua sikio langu, na sikuaasi, wala kurudi nyuma. 6Niliwapa mgongo wangu wale wanaonipiga mimi, na shavu langu kwa wale wanaopokonya nje ndevu zangu; Sitouficha uso wangu kutokana na matendo ya aibu na kutema mate. 7Maana Bwana Yahwe atanisaidia mimi; hivyo basi sitapatwa na aibu; hivyo nimeufanya uso wangu kama jiwe, maana ninajua kwamba sitaabishwa.
Wimbo wa katikati
7Wale wote wanionao hunisuta; hunidhihaki; hunitikisia vichwa vyao. 8Wao husema, “Yeye anamwamini Yahwe; mwache Yahwe amuokoe. Mwache amuokoe yeye, kwa kuwa yeye anampendeza sana Yeye.” 16Kwa maana mbwa wamenizunguka; kundi la watu waovu limenizunguka; wamenitoboa mikono yangu na miguu yangu. 17Nami ninaweza kuihesabu mifupa yangu. Wao wananitazama na kunishangaa. 18Wao wanagawa mavazi yangu kati yao wenyewe, wanapiga kura kwa ajili ya mavazi yangu. 19Usiwe mbali, Yahwe; tafadhali harakisha kunisaidia mimi, nguvu yangu! 22Nami nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu; katikati ya kusanyiko la watu nitakusifu wewe. 23Ninyi mnao mwogopa Yahwe, msifuni yeye! Ninyi nyote kizazi cha Yakobo, muheshimuni yeye! Simameni katika hofu yake, ninyi nyote kizazi cha Israeli!
Somo la pili
6Ingawaje yeye ni sawa na Mungu. Lakini hakujali kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kushikamana nacho. 7Badala yake, alijishusha mwenyewe. Alichukua umbo la mtumishi. Akajitokeza katika mfano wa wanadamu. Alionekana mwanadamu. 8Yeye alijinyeyekeza na kuwa mtii hadi kifo, kifo cha msalaba. 9Hivyo basi Mungu alimtukuza sana. Alimpa jina kuu lipitalo kila jina. 10Alifanya hivyo ili kwamba katika jina la Yesu kila goti sharti liiname. Magoti ya walio mbinguni na walio juu ya ardhi na chini ya ardhi. 11Na alifanya hivyo ili kwamba kila ulimi sharti ukiri kwamba Yesu kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.
Injili
1Ilikuwa siku mbili tu baada ya sikukuu ya Pasaka na ya Mikate Isiyotiwa Chachu. Makuhani wakuu na waandishi walikuwa wakitafuta namna ya kumkamata Yesu kwa hila na kumuua. 2Kwa kuwa walisema, “Sio wakati huu wa sikukuu, watu wasije wakafanya ghasia.” 3Wakati Yesu alipokuwa Bethania nyumbani kwa Simoni mkoma, na alipokuwa akielekea mezani, mwanamke mmoja alikuja kwake akiwa na chupa ya marashi ya nardo safi yenye gharama kubwa sana, aliivunja chupa na kuimimina juu ya kichwa chake. 4Lakini kulikuwa na baadhi yao waliokasirika. Waliambiana wao kwa wao wakisema, “Ni nini sababu ya upotevu huu? 5Manukato haya yangeweza kuuzwa kwa zaidi ya dinari mia tatu, na wakapewa maskini.” Nao walimkemea. 6Lakini Yesu alisema, “Mwacheni peke yake. Kwa nini mnamsumbua? Amefanya jambo zuri kwangu. 7Siku zote maskini mnao, na wakati wowote mnapotamani mnaweza kufanya mazuri kwao, lakini hamtakuwa nami wakati wote. 8Amefanya kile anachoweza: ameupaka mwili wangu mafuta kwa ajili ya maziko. 9Kweli nawaambia, kila mahali injili inapohubiriwa katika ulimwengu wote, kile alichofanya mwanamke huyu kitazungumzwa kwa ukumbusho wake. 10Kisha Yuda Iskariote, mmoja wa wale kumi na wawili, alikwenda kwa wakuu wa makuhani ili kwamba apate kumkabidhi kwao. 11Wakati wakuu wa Makuhani waliposikia hivyo, walifurahi na wakaahidi kumpa fedha. Alianza kutafuta nafasi ya kumkabidhi kwao. 12Katika siku ya kwanza ya mkate usiotiwa chachu, wakati walipotoa mwanakondoo wa pasaka, wanafunzi wake walimwambia, “Unataka twende wapi tukaandae ili upate kula mlo wa Pasaka?” 13Aliwatuma wanafuzi wake wawili na kuwaambia, “Nendeni mjini, na mwanamume ambaye amebeba mtungi ataonana nanyi. Mfuateni. 14Nyumba atakayoingia, mfuateni na mmwambie mwenye nyumba hiyo, 'Mwalimu asema, “Kiko wapi chumba cha wageni mahali nitakapokula Pasaka na wanafunzi wangu?” 15Atawaonesha chumba cha juu kikubwa chenye samani ambacho kiko tayari. Fanyeni maandalizi kwa ajili yetu pale.” 16Wanafunzi waliondoka wakaenda mjini; walikuta kila kitu kama alivyokuwa amewaambia, na wakaandaa mlo wa Pasaka. 17Wakati ilipokuwa jioni, alikuja na wale Kumi na wawili. 18Na walipokuwa wakiikaribia meza na kula, Yesu alisema, “Kweli nawaambia, mmoja kati yenu anayekula pamoja nami atanisaliti.” 19Wote walisikitika, na mmoja baada ya mwingine walimwambia, “Hakika siyo mimi?” 20Yesu alijibu na kuwaambia, “Ni mmoja wa Kumi na wawili kati yenu, mmoja ambaye sasa anachovya tonge katika bakuli pamoja nami. 21Kwa kuwa Mwana wa Adamu atakwenda kama vile maandiko yasemavyo juu yake. Lakini ole wake mtu yule ambaye kupitia yeye Mwana wa Adamu atasalitiwa! Ingekuwa vizuri zaidi kwake kama mtu yule asingezaliwa.” 22Na walipokuwa wakila, Yesu alichukua mkate, akaubariki, na kuumega. Aliwapa akisema, “Chukueni. Huu ni mwili wangu.” 23Alichukua kikombe, akashukuru, na akawapatia, na wote wakakinywea. 24Aliwaambia, “Hii ni damu yangu ya agano, damu imwagikayo kwa ajili ya wengi. 25Kweli nawaambia, sitakunywa tena katika zao hili la mzabibu mpaka siku ile nitakapokunywa mpya katika ufalme wa Mungu.” 26Walipokwisha kuimba wimbo, walikwenda nje katika Mlima wa Mizeituni. 27Yesu aliwaaambia, “Ninyi nyote mtajitenga mbali kwa sababu yangu, kwa kuwa imeandikwa, 'Nitampiga mchungaji na kondoo watatawanyika.' 28Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia mbele yenu Galilaya.” 29Petro alimwambia, “Hata kama wote watakuacha, mimi sitakuacha.” 30Yesu alimwambia, “Kweli nakuambia, usiku huu, kabla jogoo hajawika mara mbili, utakuwa umenikana mara tatu.” 31Lakini Petro alisema, “Hata itanilazimu kufa pamoja nawe, sitakukana.” Wote walitoa ahadi ile ile. 32Walikuja kwenye eneo lililoitwa Gethsemane, na Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati nasali.” 33Aliwachukua Petro, Yakobo, na Yohana pamoja naye, akaanza kuhuzunika na kutaabika sana. 34Aliwaambia, “Nafsi yangu ina huzuni sana, hata kufa. Bakini hapa na mkeshe.” 35Yesu alienda mbele kidogo, akaanguka chini, akaomba, kama ingewezekana, kwamba saa hii ingemwepuka. 36Alisema, “Aba, Baba, Mambo yote kwako yanawezekana. Niondolee kikombe hiki. Lakini siyo kwa mapenzi yangu, bali mapenzi yako.” 37Alirudi na kuwakuta wamelala, na akamwambia Petro, “Simoni, je umelala? Hukuweza kukesha hata saa moja? 38Kesheni na muombe kwamba msije mkaingia katika majaribu. Hakika roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.” 39Alienda tena na kuomba, na alitumia maneno yaleyale. 40Alikuja tena akawakuta wamelala, kwa kuwa macho yao yalikuwa mazito na hawakujua nini cha kumwambia. 41Alikuja mara ya tatu na kuwaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Yatosha! Saa imefika. Tazama! Mwana wa Adamu atasalitiwa mikononi mwa wenye dhambi. 42Amkeni, twendeni. Tazama, yule anayenisaliti yuko karibu.” 43Mara tu alipokuwa bado anaongea, Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili, alifika, na kundi kubwa kutoka kwa wakuu wa makuhani, waandishi na wazee wenye mapanga na marungu. 44Wakati huo msaliti wake alikuwa amewapa ishara, akisema, Yule nitakayembusu, ndiye. Mkamateni na kumpeleka chini ya ulinzi.” 45Wakati Yuda alipofika, moja kwa moja alienda kwa Yesu na kusema, “Mwalimu!” Na akambusu. 46Kisha wakumtia chini ya ulinzi na kumkamata. 47Lakini mmoja kati yao aliyesimama karibu naye alichomoa upanga wake akampiga mtumishi wa kuhani mkuu na kumkata sikio. 48Yesu aliwaambia, “Mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kama mnyang'anyi? 49Wakati kila siku nilikuwa nanyi na nikifundisha hekaluni, hamkunikamata. Lakini hili limefanyika ili maandiko yatimie. 50Na wale wote waliokuwa na Yesu walimwacha na kukimbia. 51Kijana mmoja alimfuata, aliyekuwa amevaa shuka tu aliyokuwa amejifunika kumzunguka; walimkamata lakini 52aliwaponyoka akaiacha shuka pale akakimbia uchi. 53Walimwongoza Yesu kwa kuhani mkuu. Pale walikusanyika pamoja naye makuhani wakuu wote, wazee, na waandishi. 54Petro naye alimfuata Yesu kwa mbali, kuelekea kwenye ua wa kuhani mkuu. Aliketi pamoja na walinzi, waliokuwa karibu na moto wakiota ili kupata joto. 55Wakati huo makuhani wakuu wote na Baraza lote walikuwa wakitafuta ushahidi dhidi ya Yesu ili wapate kumwua. Lakini hawakuupata. 56Kwa kuwa watu wengi walileta ushuhuda wa uongo dhidi yake, lakini hata ushahidi wao haukufanana. 57Baadhi walisimama na kuleta ushahidi wa uongo dhidi yake; wakisema, 58“Tulimsikia akisema, 'Nitaliharibu hekalu hili lililotengenezwa kwa mikono, na ndani siku tatu nitajenga lingine lisilotengenezwa kwa mikono.'” 59Lakini hata ushahidi wao haukufanana. 60Kuhani mkuu alisimama katikati yao na akamwuliza Yesu, “Je, huna jibu? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?” 61Lakini alikaa kimya na hakujibu chochote. Mara Kuhani mkuu alimwuliza tena, “Je wewe ni Kristo, mwana wa Mbarikiwa?” 62Yesu alisema, “Mimi ndiye. Na utamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kulia wa nguvu akija na mawingu ya mbinguni.” 63Kuhani mkuu alirarua mavazi yake na kusema, “Je, bado tunahitaji mashahidi? 64Mmesikia kufuru. Uamuzi wenu ni upi?” Na wote walimhukumu kama mmoja aliyestahili kifo. 65Baadhi wakaanza kumtemea mate na kumfunika uso na kumpiga na kumwambia, “Tabiri!” Maafisa walimchukua na kumpiga. 66Na Petro alipokuwa bado yuko chini uani, mtumishi mmoja wa wasichana wa kuhani mkuu alikuja kwake. 67Alimwona Petro alipokuwa amesimama akiota moto, na alimtazama kwa kumkaribia. Kisha alisema, “Nawe pia ulikuwa na Mnazareti, Yesu”. 68Lakini alikataa, akisema, “Sijui wala sielewi kuhusu kile unachosema!” Kisha alitoka akaenda nje uani. 69Lakini mtumishi wa kike pale, alimwona na alianza kuwaambia tena wale ambao walikuwa wamesimama pale, “Mtu huyu ni mmoja wao!” 70Lakini alikana tena. Baadaye kidogo wale waliokuwa wamesimama pale walikuwa wakimwambia Petro, “Hakika wewe ni mmoja wao, kwa maana wewe pia ni Mgalilaya.” 71Lakini alianza kujiweka mwenyewe chini ya laana na kuapa, “Simjui mtu huyu mnayemsema.” 72Kisha jogoo aliwika mara ya pili. Kisha Petro alikumbuka maneno ambayo Yesu aliyokuwa amemwambia: “Kabla jogoo hajawika mara mbili, utanikana mara tatu.” Na alianguka chini na kulia. 15:1Asubuhi na mapema wakuu wa makuhani walikutana pamoja na wazee na waandishi na baraza zima la wazee. Kisha wakamfunga Yesu wakampeleka kwa Pilato. Pilato akamwuliza, “wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” 2“Akamjibu, “Wewe umesema hivyo.” 3Wakuu wa makuhani wakaeleza mashitaka mengi juu ya Yesu. 4Pilato akamwuliza tena, “Hujibu chochote? Huoni jinsi wanavyokushtaki kwa mambo mengi? 5Lakini Yesu hakumjibu Pilato, na hiyo ilimshangaza. 6Kwa kawaida wakati wa sikukuu humfungulia mfungwa mmoja, mfungwa waliyemwomba. 7Kulikuwapo wahalifu gerezani, miongoni mwa wauaji kati ya walioasi wanaotumikia makosa yao. Alikuwepo mtu mmoja aitwaye Baraba. 8Umati ulikuja kwa Pilato, na kumwomba afanye kama alivyofanya huko nyuma. 9Pilato akawajibu na kusema, “Mnataka niwafungulie Mfalme wa Wayahudi?” 10Kwa kuwa alijua ni kwa sababu ya wivu wakuu wa makuhani walimkamata Yesu na kumleta kwake. 11Lakini wakuu wa makuhani walichochea umati kupiga kelele kwa sauti kwamba afunguliwe Baraba badala yake. 12Pilato akawajibu tena na kusema, “Nimfanye nini Mfalme wa Wayahudi? 13Wakapiga kelele tena, “Msulibishe!” 14Pilato akasema, “Amefanya jambo gani baya?” Lakini wakazidi kupiga kelele zaidi na zaidi “Msulibishe.” 15Pilato akitaka kuwaridhisha umati, akawafungulia Baraba. Akampiga Yesu mijeledi kisha akamtoa ili asulibiwe. 16Askari walimwongoza hadi ndani ya ua (ule ulio ndani ya kambi) na walikusanyika pamoja kikosi cha askari. 17Wakamvika Yesu kanzu ya rangi ya zambarau, na wakasokota taji ya miiba wakamvika. 18Wakaanza kumdhihaki na kusema, “Salam, Mfalme wa Wayahudi!” 19Wakampiga kichwani kwa mwanzi na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake kwa kumheshimu. 20Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua ile kanzu ya rangi ya zambarau na kumvika mavazi yake, na wakamtoa nje kwenda kumsulibisha. 21Wakamlazimisha mpita njia kumsaidia, aliyekuwa anaingia mjini kutoka shamba. Aitwaye Simoni Mkirene (baba yake Iskanda na Rufo); wakamlazimisha kubeba msalaba wa Yesu. 22Askari wakampeleka Yesu mahali paitwapo Goligotha (maana ya tafsiri hii ni, Sehemu ya Fuvu la kichwa). 23Wakampa mvinyo iliyochanganywa na manemane, lakini hakunywa. 24Wakamsulibisha na wakagawana mavazi yake, wakayapigia kura kuamua kipande atakachopata kila askari. 25Yapata saa tatu asubuhi walipomsulibisha. 26Wakaweka juu yake ubao ulioandikwa shitaka, “Mfalme wa Wayahudi.” 27Walimsubisha pamoja na majambazi wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine kushoto kwake. 29Nao waliokuwa wakipita walimtukana, wakitikisa vichwa vyao wakisema, “Aha! wewe utakayevunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, 30jiokoe mwenyewe na ushuke chini toka msalabani!” 31Kwa namna ile ile wakuu wa makuhani walimdhihaki wakisemezana, pamoja na waandishi na kusema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe. 32Kristo Mfalme wa Israel, shuka chini sasa toka msalabani, ili tuweze kuona na kuamini.” Na wale waliosulubiwa pamoja naye pia walimdhihaki. 33Ilipofika saa sita, giza likaja juu ya nchi yote hadi saa tisa. 34Wakati wa saa tisa, Yesu alipiga kelele kwa sauti kubwa, “Eloi, Eloi, lama sabaktani?” ikiwa na maana “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha?” 35Baadhi ya hao waliosimama waliposikia wakasema, “Tazama, anamwita Eliya.” 36Mtu mmoja akakimbia, akajaza siki katika sponji na kuiweka juu ya mti wa mwanzi, akampa ili anywe. Mtu mmoja akasema, “Ngoja tuone kama Eliya atakuja kumshusha chini.” 37Kisha Yesu akalia kwa sauti kubwa na akafa. 38Pazia la hekalu likagawanyika vipande viwili toka juu mpaka chini. 39Ofisa mmoja aliyekuwa amesimama akimwelekea Yesu, alipoona amekufa kwa jinsi ile, akasema, “Kweli huyu mtu alikuwa Mwana wa Mungu.” 40Walikuwepo pia wanawake waliokuwa wakitazama kwa mbali. Miongoni mwao alikuwepo Mariamu Magdalena, Mariamu (mama yake Yakobo mdogo wa Yose), na Salome. 41Wakati alipokuwa Galilaya walimfuata na kumtumikia. Na wanawake wengine wengi pia waliambatana naye hadi Yerusalemu. 42Kulipokuwa jioni, na kwa kuwa ilikuwa siku ya maandalio, siku kabla ya Sabato, 43Yusufu wa Arimathaya alikuja pale. Alikuwa ni mjumbe wa Baraza anayeheshimiwa mtu anayeutarajia Ufalme wa Mungu. Kwa ujasiri akaenda kwa Pilato, na kuuomba mwili wa Yesu. 44Pilato akashangazwa kwamba Yesu tayari amekufa; akamwita yule afisa akamwuliza kama Yesu amekufa. 45Alipopata uhakika kwa afisa kwamba amekufa, alimruhusu Yusufu kuuchukua mwili. 46Yusufu alikuwa amenunua sanda. Akamshusha toka msalabani, akamfunga kwa sanda, na kumweka ndani ya kaburi lililochimbwa katika mwamba. Kisha akalivingirisha jiwe mlangoni mwa kaburi. 47Mariamu Magdalena na Mariamu mama yake Yose waliona sehemu alipozikwa Yesu.
Kalenda ya Jumla ya Kirumi; baraza la maaskofu linaweza kuhamisha baadhi ya maadhimisho (Epifania, Kupaa Bwana, Ekaristi Takatifu) hadi Jumapili au kuongeza yake. Kitabu cha masomo: mzunguko wa Jumapili B, mwaka wa siku za kazi I.
Vyanzo: Swahili Unlocked Literal Bible · © Door43 World Missions Community, CC BY-SA 4.0 · Vyanzo na haki