Bible Explorer

Gundua › Injili kando kwa kando › Mateso

Injili kando kwa kando · Mateso

Gethsemane

Mt 26:36–46 · Mk 14:32–42 · Lk 22:39–46

Mathayo

Mt 26:36–46

36Baadaye Yesu alienda nao mahali panapoitwa Gethsemane na aliwaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati nikienda huko na kuomba.”

37Akamchukua Petro na wana wawili wa Zebedayo na akaanza kuhuzunika na kusononeka.

38Kisha aliwaambia, “Roho yangu ina huzuni kubwa sana, hata kiasi cha kufa. Bakini hapa na mkeshe pamoja nami.”

39Akenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, na kuomba. Akasema, “Baba yangu, kama inawezekana, kikombe hiki kiniepuke. Isiwe kama ninavyotaka mimi, bali kama utakavyo wewe.”

40Akawaendea wanafunzi na akawakuta wamelala usingizi, na akamwambia Petro, “Kwa nini hamkuweza kukesha nami kwa saa moja?

41Kesheni na kuomba kusudi msiingie majaribuni. Roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”

42Akaenda zake mara ya pili na kuomba, akasema, “Baba yangu, kama jambo hili haliwezi kuepukika na ni lazima nikinywee kikombe hiki, mapenzi yako yatimizwe.”

43Akarudi tena na kuwakuta wamelala usingizi, kwa kuwa macho yao yalikuwa mazito.

44Kisha akawaacha tena akaenda zake. Akaomba mara ya tatu akisema maneno yaleyale.

45Baadaye Yesu aliwaendea wanafunzi wake na kuwaambia, “Bado mmelala tu na kujipumzisha? Tazameni, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anasalitiwa mikononi mwa wenye dhambi.

46Amkeni, tuondoke. Tazama, yule anaye nisaliti amekaribia.”

Marko

Mk 14:32–42

32Walikuja kwenye eneo lililoitwa Gethsemane, na Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Kaeni hapa wakati nasali.”

33Aliwachukua Petro, Yakobo, na Yohana pamoja naye, akaanza kuhuzunika na kutaabika sana.

34Aliwaambia, “Nafsi yangu ina huzuni sana, hata kufa. Bakini hapa na mkeshe.”

35Yesu alienda mbele kidogo, akaanguka chini, akaomba, kama ingewezekana, kwamba saa hii ingemwepuka.

36Alisema, “Aba, Baba, Mambo yote kwako yanawezekana. Niondolee kikombe hiki. Lakini siyo kwa mapenzi yangu, bali mapenzi yako.”

37Alirudi na kuwakuta wamelala, na akamwambia Petro, “Simoni, je umelala? Hukuweza kukesha hata saa moja?

38Kesheni na muombe kwamba msije mkaingia katika majaribu. Hakika roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”

39Alienda tena na kuomba, na alitumia maneno yaleyale.

40Alikuja tena akawakuta wamelala, kwa kuwa macho yao yalikuwa mazito na hawakujua nini cha kumwambia.

41Alikuja mara ya tatu na kuwaambia, “Bado mmelala na kupumzika? Yatosha! Saa imefika. Tazama! Mwana wa Adamu atasalitiwa mikononi mwa wenye dhambi.

42Amkeni, twendeni. Tazama, yule anayenisaliti yuko karibu.”

Luka

Lk 22:39–46

39Baada ya chakula cha usiku, Yesu aliondoka, kama ambavyo amekuwa akifanya mara kwa mara, akaenda mlima wa Mzeituni, na wanafunzi wakamfuata.

40Walipofika, aliwaambia, “Ombeni kwamba msiingie majaribuni.”

41Akaenda mbali na wao kama mrusho wa jiwe, akapiga magoti akaomba,

42akisema, “Baba, kama unataka, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nitakavyo mimi, lakini mapenzi yako yafanyike.”

43Kisha malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu.

44Akiwa katika kuugua, akaomba kwa dhati zaidi, na jasho lake likawa kama matone makubwa ya damu yakidondoka chini.

45Wakati alipoamka kutoka katika maombi yake, alikuja kwa wanafunzi, na akawakuta wamelala kwa sababu ya huzuni yao,

46na akawauliza, “Kwanini mnalala? Amkeni muombe, kwamba msiingie majaribuni.”

Yamewekwa alama: maneno yaliyo katika masimulizi yote, katika tafsiri unayosoma. Maneno ya kawaida zaidi (“na”, “yeye”) hayawekwi alama; neno katika umbo jingine huenda lisiwekwe.

Swahili Unlocked Literal Bible · Sambamba zimechaguliwa kwa mkono kutoka maandiko na kulinganishwa na marejeo ya OpenBible.info (CC BY). Kando kwa kando huwekwa tukio au neno lilelile tu. OpenBible.info · CC BY