18Kisha mfalme Daudi akaingia ndani na kuketi mbele ya Yahwe; akasema, “Mimi ni nani, Yahwe Mungu, na familia yangu ni nini hata umenileta hapa nilipo?
19Na hili lilikuwa jambo dogo mbele yako, Bwana Yahwe. Hata ukasema kuhusu familia ya mtumishi wako wakati mkuu ujao, nawe umenionesha vizazi vijavyo, Bwana Yahwe!
20Mimi Daudi, niseme nini zaidi kwako? Umemweshimu mtumishi wako, Bwana Yahwe.
21Kwa ajili ya neno lako, na kwa ajili ya kutimiza kusudi lako mwenyewe, umefanya jambo kubwa namna hii na kulidhihirisha kwa mtumishi wako.
22Kwa hiyo wewe ni mkuu, Bwana Yahwe. Kwa maana hakuna mwingine aliye kama wewe, na hakuna Mungu mwingine badala yako, kama jinsi ambayo tumesikia kwa masikio yetu wenyewe.
23Kwani kuna taifa lipi lililo kama watu wako Israeli, taifa moja juu ya nchi ambalo wewe, Mungu, ulikwenda na kuwakomboa kwa ajili yako wewe mwenyewe? Ulifanya hivi ili kwamba wawe watu kwa ajili yako mwenyewe, kujifanyia jina kwa ajili yako mwenyewe, na kufanya matendo makuu na ya kuogofya kwa ajili ya nchi yako. Uliyaondoa mataifa na miungu yao kutoka mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri.
24Umeiimarisha Israel kama watu wako daima, na wewe, Yahwe, kuwa Mungu wao.
25Basi sasa, Yahwe Mungu, ahadi uliyofanya kuhusu mtumishi wako na familia yake iwe imara daima. Ufanye kame uilivyo sema.
26Na jina lako liwe kuu daima, ili watu waseme, 'Yahwe wa majeshi ni Mungu wa Israeli,' wakati nyumba yangu, Daudi, mtumishi wako itakapokaa imara mbele zako daima.
27Kwa maana wewe, Yahwe wa majeshi, Mungu wa Israeli, umedhihirisha kwa mtumishi wako kwamba utamjengea nyumba. Ndiyo maana mimi, mtumishi wako, nimepata ujasiri kuomba kwako.
28Sasa, Bwana Yahwe, wewe ni Mungu, na maneno yako ni amini, na umefanya ahadi hii njema kwa mtumishi wako.
29Sasa basi, na ikupendeze kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili iendelee mbele yako daima. Kwa maana wewe, Bwana Yahwe, umeyasema mambo haya, na kwa ahadi yako nyumba ya mtumishi wako itabarikiwa daima.