Mwanzo › Masomo ya Biblia ya kila siku › Machi 2027 › 11 Machi
Kalenda ya Kiorthodoksi · 26 Februari (kalenda ya Juliani)
Masomo ya Kiorthodoksi ya siku — 11 Machi 2027
Alhamisi · Wiki ya Kuacha Jibini · Sauti ya 7
Sikukuu na watakatifu
Alhamisi ya Wiki ya Kuacha Jibini
Wiki ya Kuacha Jibini
Bila nyama; maziwa, mayai na samaki vinaruhusiwa
Hivi ndivyo kwa kanuni ya kimonaki. Parokiani, kipimo cha mfungo huamuliwa pamoja na baba wa kiroho, kulingana na afya, umri na hali.
Masomo ya siku
Waraka
11Ole wao! Kwa kuwa wametembea katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu. Wameangamia katika uasi wa Kora. 12Hawa ni miamba katika sherehe zenu za upendo, wakisherehekea bila aibu, wakijilisha tu wenyewe. Ni mawingu yasiyo na maji, yanayobebwa na upepo, ni miti iliyopukutika isiyo na matunda iliyo kufa mara mbili, iliyong'olewa mizizi 13Ni mawimbi ya bahari yenye kelele yakitoa aibu yao wenyewe, Ni nyota zinazorandaranda ambazo weusi wa giza umetunzwa kwa ajili yao milele. 14Enoko, wa saba katika orodha ya Adamu, alitabiri kuhusu wao, akisema, “Tazama! Bwana anakuja na maelfu kwa maelfu ya watakatifu wake, 15ili afanye hukumu juu ya kila mtu, na kutia hatia wote wasiomcha Mungu juu ya matendo yao yote waliyokwishafanya katika njia zisizo za kitauwa, na kwa maneno yote ya ukali ambayo wasio watauwa wameyanena dhidi yake.” 16Hawa ni wale wanung'unikao, walalamikao ambao hufuata tamaa zao za uovu, wajivunao mno, ambao kwa faida yao hudanganya wengine. 17Lakini ninyi, wapenzi, kumbukeni maneno ambayo yalinenwa zamani na mitume wa Bwana Yesu Kristo. 18Walisema kwenu, “Katika wakati wa mwisho kutakuwa na watu wanaodhihaki ambao hufuata tamaa zao zisizo za kitauwa.” 19Watu hawa ni watenganishaji, wanatawaliwa na tamaa za asili, na hawana Roho. 20Lakini ninyi, wapenzi, kama mjijengavyo katika imani yenu takatifu sana, na kama muombavyo katika Roho Mtakatifu, 21jitunzeni katika upendo wa Mungu, na msubiri rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ambayo huwapatia uzima wa milele. 22Onesheni rehema kwa wale walio na shaka. 23Waokoeni wengine kwa kuwanyakua kutoka katika moto. Kwa wengine onesheni huruma kwa hofu, mkichukia hata vazi lililotiwa doa na mwili. 24Sasa kwake awezaye kuwalinda msijikwae, na kuwasababisha msimame mbele ya utukufu wake, bila mawaa na kuwa na furaha kuu, 25kwake Mungu pekee mwokozi kupitia Yesu Kristo Bwana wetu, utukufu uwe kwake, ukuu, uwezo na nguvu kabla ya nyakati zote, na sasa na hata milele. Amina.
Injili
1Mkutano wote wakasimama, wakampeleka Yesu mbele ya Pilato. 2Wakaanza kumshutumu, wakisema, “Tumemkuta mtu huyu akipotosha taifa letu, kwa kukataza tusitoe kodi kwa Kaisari, na akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, Mfalme.” 3Pilato akamuuliza, akisema, “Je wewe ni Mfalme wa Wayahudi?” Na Yesu akamjibu akisema, “Wewe wasema hivyo”. 4Pilato akamuambia kuhani mkuu na makutano, “Sioni kosa kwa mtu huyu”. 5Lakini wao wakasisitiza, wakisema, “ Amekuwa akiwachochea watu, akifundisha katika Uyahudi yote, kuanzia Galilaya na sasa yuko hapa.” 6Pilato aliposikia haya, akaulizia kama mtu huyo ni wa Galilaya? 7Alipotambua kuwa alikuwa chini ya utawala wa Herode, akampeleka Yesu kwa Herode, ambaye naye alikuwa Yerusalemu kwa siku hizo. 8Herode alipomuona Yesu, alifurahi sana kwasababu alitaka kumuona kwa siku nyingi. Alisikia habari zake na alitamani kuona moja ya miujiza ikifanywa na yeye. 9Herode alimhoji Yesu kwa maneno mengi, lakini Yesu hakumjibu chochote. 10Makuhani wakuu pamoja na waandishi walisimama kwa ukali wakimshitaki. 11Herode pamoja na maaskari wake, walimtukana na kumdhihaki, na kumvika mavazi mazuri, kisha akamrudisha Yesu kwa Pilato. 12Herode na Pilato wakawa marafiki kuanzia siku hiyo, (kabla ya hapo walikuwa maadui). 13Pilato akawaita pomoja makuhani wakuu na watawala na umati wa watu, 14Akawaambia, “Mmeniletea mtu huyu kama mtu anaye waongoza watu wafanye mabaya, na tazama, baada ya kuwa nimemhoji mbele yenu, sikuona kosa kwa mtu huyu kuhusu mambo yote ambayo ninyi mnamshitaki yeye. 15Hapana, wala Herode, kwa maana amemrudisha kwetu, na tazama hakuna chochote alichokifanya kinachostahili adhabu ya kifo. 16Kwahiyo basi nitamuadhibu na kumuachilia. 17(Sasa, Pilato anawajibika kumuachilia mfungwa mmoja kwa wayahudi wakati wa sikukuu). 18Lakini wote wakapiga kelele pamoja, wakisema, “Mwondoe huyo, na tufungulie Baraba!” 19Baraba alikuwa ni mtu ambaye amewekwa gerezani kwa sababu ya uasi fulani katika jiji na kwa kuua. 20Pilato akawaambia tena, akitamani kumwachilia Yesu. 21Lakini wao wakapiga kelele, wakisema, “Msulibishe, msulibishe.” 22Akawauliza kwa mara ya tatu, “kwa nini, huyu mtu amefanya maovu gani? Sikupata kosa linalostahili adhabu ya kifo kwake. Kwahiyo nitakapo maliza kumuadhibu nitamuachilia.” 23Lakini wakasisitiza kwa sauti ya juu, wakitaka asulubiwe. Na sauti zao zikamshawishi Pilato. 24Hivyo Pilato akaamua kuwapatia matakwa yao. 25Akamuachilia yule waliyemtaka ambaye alifungwa kwa kusababisha ghasia na kuua. Lakini akamtoa Yesu kwa matakwa yao. 26Walipokuwa wakimpeleka, walimkamata mtu mmoja aitwaye Simoni wa Ukirene, akitokea katika nchi, wakamtwika msalaba ili abebe, akimfuata Yesu. 27umati mkubwa wa watu, na wanawake ambao walihuzunika na kuomboleza kwa ajili yake, walikuwa wakimfuata. 28Lakini akawageukia, Yesu akawaambia, 'Mabinti wa Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni ninyi wenyewe na kwa ya ajili watoto wenu. 29Tazama, siku zinakuja ambazo watasema, “Wamebarikiwa walio tasa na matumbo yasiyozaa, na matiti ambayo hayakunyonyesha. 30Ndipo watakapo anza kuiambia milima, 'Tuangukieni,' na vilima, 'Mtufunike.' 31Maana kama wakifanya mambo haya ikiwa mti mbichi, itakuwaje ukiwa mkavu?” 32wanaume wengine, wahalifu wawili, walipelekwa pamoja naye ili wauwawe. 33Walipofika mahali paitwapo Fuvu la kichwa, ndipo wakamsulubisha pamoja na wale wahalifu, mmoja upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto. 34Yesu alisema, “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. “Nao wakapiga kura, kugawa mavazi yake. 44Hapo ilikuwa karibu saa ya sita, giza likaja juu ya nchi yote hadi saa ya tisa, 45Mwanga wa jua ulizimika. Kisha pazia la hekalu likagawanyika katikati kuanzia juu. 46Akilia kwa sauti kuu, Yesu alisema, “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu,” baada ya kusema haya, akafa. 47Wakati Akida alipoona yaliyotendeka alimtukuza Mungu akisema, “Hakika huyu alikuwa mtu mwenye haki.” 48Wakati umati wa watu waliokuja pamoja kushuhudia walipoona mambo yaliyofanyika, walirudi huku wakipiga vifua vyao. 49Lakini marafiki zake, na wanawake waliomfuata toka Galilaya, walisimama kwa mbali wakiangalia hayo mambo. 50Tazama, palikuwepo na mtu aitwaye Yusufu, ambaye ni mmoja wa baraza, mtu mzuri na mwenye haki, 51(alikuwa hajakubaliana na maamuzi au matendo yao), kutoka Armathaya, mji wa Kiyahudi, ambao ulikua ukisubiria ufalme wa Mungu. 52Mtu huyu, alimkaribia Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. 53Alimshusha, na akauzungushia sanda, na akaumweka katika kaburi lililokuwa limechongwa katika jiwe, ambalo hakuna aliyewahi kuzikwa. 54Ilikuwa ni siku ya maandalizi, na Sabato inakaribia. 55Wanawake, waliokuja nao kutoka Galilaya, walimfuata, na wakaona kaburi na jinsi mwili wake ulivyolazwa. 56Walirudi na kuanza kuandaa manukato na marashi. Kisha siku ya sabato walipumzika kwa mujibu wa sheria.
Watakatifu wa siku
- Askofu Mtakatifu Porfirio, Askofu Mkuu wa Gaza (420)
- Mfiadini wa Kikasisi Petro, padri (1930)
- Mfiadini wa Kikasisi Sergio, padri (1933)
- Mtawa Mfiadini Ana (1937)
- Wafiadini wa Kikasisi Yohana, Askofu wa Rylsk, na Yohana, padri (1938)
- Mtakatifu Mtawa Sebastiani wa Sokhot, wa Poshekhonye (karibu 1500)
- Wafiadini Sebastiani na Kristodulo (karibu 66)
Tarehe zinafuata kalenda ya Juliasi ya Kanisa la Urusi (kama Makanisa ya Serbia na Georgia na Mlima Athos): 26 Februari katika kalenda ya kanisa ni 11 Machi katika kalenda ya kiraia. Makanisa ya kalenda mpya (Ugiriki, Romania, Bulgaria, Ukraine…) huadhimisha sikukuu zisizohamishika na watakatifu katika tarehe ya kiraia yenyewe, siku 13 mapema, na baadhi ya masomo yao ni tofauti; Pasaka na siku zinazoitegemea ni zilezile.
Vyanzo: Swahili Unlocked Literal Bible · © Door43 World Missions Community, CC BY-SA 4.0 · Vyanzo na haki