1Katika siku zile Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri katika nyika ya Yuda akisema,
2“Tubuni kwa maana ufalme wa mbinguni u karibu.”
3Kwa maana huyu ndiye aliyenenwa na nabii Isaya akisema, “sauti ya mtu aitaye kutoka jangwani; 'wekeni tayari njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake.”'
4Sasa Yohana alivaa manyoya ya ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni.
5Kisha Yerusalemu, Yuda yote, na eneo lote linalozunguka mto Yorodani wakaenda kwake.
6Walikuwa wakibatizwa naye katika mto Yorodani huku wakitubu dhambi zao.
7Lakini alipowaona wengi wa mafarisayo na masadukayo wakija kwake kubatizwa, akawaambia, ''Enyi uzao wa nyoka wenye sumu nani aliye waonya kuikimbia ghadhabu inayokuja?
8Zaeni matunda yaipasayo toba.
9Na msifikiri na kusemezana miongoni mwenu, 'Tunaye Ibrahimu kama baba yetu.' Kwa kuwa nawaambieni Mungu anaweza kumwinulia Ibrahimu watoto hata kutoka katika mawe haya.
10Tayari shoka limekwisha kuwekwa kwenye mzizi wa miti. Kwahiyo kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa kwenye moto.
11Ninawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba. Lakini yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi nami sistahili hata kubeba viatu vyake. Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.
12Na pepeto lake li mkononi mwake kusafisha kabisa uwanda wake na kuikusanya ngano yake ghalani. Lakini atayachoma makapi kwa moto ambao hauwezi kuzimika.